Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Yawasilishwa Bungeni
27 Jun, 2025
Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Yawasilishwa Bungeni

Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Yawasilishwa Bungeni

Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imewasilishwa rasmi Bungeni leo, tarehe 26 Juni 2025, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kupanga mustakabali wa maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, akiambatana na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Tausi Kida, waliwasilisha rasmi Rasimu hiyo mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma.

Rasimu hiyo imefikia hatua hiyo baada ya kukamilika kwa mchakato wa ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wananchi kupitia vikao, mijadala, na mikutano na makundi mbalimbali ya kijamii, wadau wa maendeleo, pamoja na wataalamu kutoka sekta tofauti.

Akizungumza mara baada ya kuwasilisha Rasimu hiyo, Prof. Mkumbo alisema Dira ya Maendeleo 2050 inalenga kuwa nyenzo kuu ya kutoa mwelekeo wa taifa katika nyanja zote za maendeleo kwa kipindi cha miaka 25 ijayo. "Tumeshirikisha Watanzania kutoka makundi yote kuhakikisha Dira hii inaakisi matarajio ya wengi," alisema.

Kabla ya kuwasilishwa Bungeni, Rasimu hiyo ilijadiliwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri, hatua inayotoa uzito na uhalali wa kisera katika mchakato huo.

Dira hiyo inatazamiwa kuwa msingi wa mipango yote ya maendeleo kwa kipindi kijacho, ikisisitiza maendeleo jumuishi, uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na teknolojia, ulinzi wa mazingira, na ustawi wa watu wote.

Uzinduzi rasmi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 umepangwa kufanyika tarehe 17 Julai 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hatua hii inaonesha dhamira ya serikali katika kuweka msingi thabiti wa maendeleo endelevu, yenye kuzingatia changamoto na fursa za sasa na zijazo.