TUME YAKUTANA NA WATAFITI NCHINI KUJADILI NAMNA YA KUOANISHA TAFITI KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA 2050
TUME YAKUTANA NA WATAFITI NCHINI KUJADILI NAMNA YA KUOANISHA TAFITI KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA 2050
Tume ya Taifa ya Mipango imeanza kuweka mkakati wa kuhakikisha tafiti zinakuwa msingi wa upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini.
Mkakati huo unalenga kuunganisha nguvu za taasisi za utafiti ili matokeo yake yasaidie kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza na wadau wa utafiti jijini Dodoma, Machi 23, 2026, Katibu Mkuu (Mipango) na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Dkt. Tausi Kida, alisema dhamira ya serikali ni kuwa na mfumo rasmi utakaofanya tafiti ziwe na matokeo yanayoonekana mchakato wa maendeleo ya Taifa.
"Tunajielekeza kuanza utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo (FYDP IV) kama hatua ya kwanza ya utekelezaji wa Dira 2050. Hivyo, Ajenda ya Taifa ya Utafiti (2026/27–2030/31) ni nyenzo muhimu katika safari hii," alisema Dkt. Kida.
Ili kufanikisha hilo, Tume imeanza kwa kufanya kikao cha mashauriano na taasisi za tafiti nchini kutoka sekta binafsi na sekta ya umma, ikiwa ni hatua ya kuoanisha ajenda za tafiti katika utekelezaji wa Dira 2050.
Aidha, pamoja na mambo mengine, Dkt. Kida amebainisha kuwa Tume itaanzisha kanzi-data ya tafiti, Mfumo utakaosaidia: Kusimamia shughuli zote za utafiti nchini, Kuhifadhi ripoti za matokeo ya tafiti, na kuishauri serikali kufanya maamuzi yenye ushahidi wa kitaalamu.