UNDP ioanishe mikakati ya ushirikiano na vipaumbele vya kitaifa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Mbaga Kida, amekutana na kufanya mazungumzo na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Tanzania.
Majadiliano baina ya pande hizo mbili yamefanyika leo jijini Dar es Salaam na kuhudhiriwa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara kwa njia ya Mtandao akiwa Tokyo-Japan ambapo yamegusia kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya upangaji, ufuatiliaji na tathmini ya maendeleo.
“Kuna umuhimu wa kuoanisha mfumo wa ushirikiano wa maendeleo wa UNDP na vipaumbele vya kitaifa hasa kwa kuangalia Dira ya Maendeleo 2050, Mpango wa Muda Mrefu (LTPP), na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP VI)” Alisema Dkt. Kida.
Aidha, viongozi hao walisisitiza kuimarisha uchambuzi wa umaskini na tofauti za kijamii, kufufua Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu, kuunganisha tafiti na utungaji wa sera, pamoja na kujenga uwezo wa taasisi katika ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha utekelezaji wenye matokeo chanya.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania Bw. Shigeki Komatsubara amesema kuwa Shirika hilo linatambua mchango mkubwa wa Tume ya Taifa ya Mipango katika kusukuma ajenda za maendeleo ya nchi, na kuahidi kuendelea kutumia mitandao ya kikanda na kimataifa kuunga mkono juhudi hizo.
Aidha, Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Watendaji wa Tume: Dkt. Mursali Milanzi (Mipango ya Kitaifa), Dkt. Blandina Kilama (Biashara na Ubunifu) na Bw. Sosthenes Kewe (Utendaji na Tathmini), kwa upande wa Tume ya Taifa ya Mipango na kwa upande wa UNDP waliwakilishwa na Bw. Godfrey Mulisa, Mkuu wa Ofisi ya UNDP Dodoma; Bi. Agnes Arrey-Etta, Afisa Ushirikiano.