Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

Dkt. Fred Msemwa
Fred Msemwa photo
Dkt. Fred Msemwa
Katibu Mtendaji

Barua pepe: es@planning.go.tz

Simu: 026-2961722

Wasifu

Fred Msemwa ni kiongozi makini, mwenye ujuzi wa hali ya juu wa kiufundi na mtazamo wa kijasiriamali. Amefanya kazi katika sekta mbalimbali zikiwemo mali isiyohamishika, ardhi na ujenzi, utalii, mafuta, gesi asilia, benki, huduma za maji, kilimo na elimu. Ameshirikiana na timu zenye kasi kubwa za utendaji na kustawi katika mazingira yenye tamaduni tofauti tofauti.

Akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 16 kama kiongozi wa biashara katika sekta ya ujenzi na mali isiyohamishika ameweza kujenga msingi thabiti wa kukabiliana na changamoto za kiuongozi zinazojitokeza. Alianza kazi kama Mhasibu na kupanda ngazi za kiuongozi hadi kuwa Meneja wa Fedha katika Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuanzia mwaka 1999 hadi 2005, kisha akateuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii. Hivi karibuni, alihudumu kama Mtendaji Mkuu wa Kwanza wa Watumishi Housing Investments (WHI), ambako aliongoza timu kuijenga WHI kuwa miongoni mwa kampuni kubwa ya uendelezaji wa makazi na usimamizi wa fedha hapa Tanzania.

Akiwa WHI, Dkt. Msemwa aliongoza kwa mafanikio ujenzi wa zaidi ya nyumba 1,000 za gharama nafuu kwa ajili ya watumishi wa umma, kuwawezesha kumiliki nyumba. Aidha, alianzisha Mfuko wa FAIDA, ambao ni mpango wa pamoja wa uwekezaji, uliolenga kuwawezesha Watanzania wa kipato cha kawaida kushiriki katika masoko ya fedha. Mfuko huo ulisajili zaidi ya wawekezaji 9,000 na uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 45. Kwa kuzingatia ni kwamba, mauzo ya awali ya hisa yalizidi matarajio kwa asilimia 173, ambapo Shilingi bilioni 12.95 zilikusanywa dhidi ya lengo la Shilingi bilioni 7.5.  Mfuko FAIDA  umewavutia wawekezaji wadogo kwa kuwawezesha kuwekeza kuanzia Shilingi 5,000, hivyo kukuza ujumuishaji wa kifedha kwa watu waliokuwa wakitengwa.

Fred Msemwa alihitimu katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM), ana Shahada ya Uzamili ya Fedha (MBA in Finance), Shahada ya Uzamivu ya Utawala wa Biashara (PhD in Business Administration) na ni Mhasibu wa Umma aliyehitimu na kusajiliwa (FCPA). Ana uzoefu mkubwa katika ukaguzi wa mahesabu ambapo kati ya mwaka 2008 hadi 2013, alihudumu kama Mkurugenzi wa Ukaguzi katika Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ambapo aliongoza kuanzishwa kwa mifumo imara ya udhibiti wa ndani, usimamizi wa vihatarishi, na utawala bora ndani ya taasisi hiyo. Pia amewahi kuwa mshirika katika kampuni ya MGK Consult inayotoa huduma za ukaguzi, kodi na ushauri wa kitaalamu.

Katika sekta ya benki, Dkt. Msemwa amewahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya TIB Corporate Bank na CRDB Bank Plc, pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa CRDB DRC. Aidha, amehudumu katika bodi za NBAA, SAGCOT, DAWASA na BRELA.

Tarehe 27 Februari 2025, aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC) akiwa na jukumu la kusimamia usimamizi wa uchumi, kukuza sekta binafsi, kuandaa mipango ya kitaifa ya maendeleo ya muda  mrefu, ya kati na muda mfupi, pamoja na kuratibu utekelezaji wake katika sekta zote.

Fred pia ni mwandishi wa kitabu kiitwacho Usimamizi wa Biashara na Fedha, na ni Mwenyekiti wa kujitolea wa Taasisi ya Youth Dreams Foundation (YDF), inayofundisha vijana namna ya kuanzisha na kuendeleza biashara, pamoja na mambo mengine.