Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

Katibu Mtendaji azindua uandaaji wa Mpango wa Maendelea wa miaka mitano
23 Aug, 2025
Katibu Mtendaji azindua uandaaji wa Mpango wa Maendelea wa miaka mitano

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dkt. Fred Msemwa, amezindua rasmi maandalizi ya Mpango wa Nne wa Maendaleo wa Miaka Mitano, unaohusisha wataalamu 27 wenye uzoefu katka masuala ya mipango na maendeleo.
 

Ikiwa chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi  (WCF), Dkt. John Mduma, timu hiyo inajumuisha wataalamu kutoka wizara zote za kisekta, sekta binafsi na asasi za kiraia. Kikao cha awali cha kazi hii kilifanyika Dar es Salaam tarehe 18/8/2025, kikiwa ni miongoni mwa nyenzo muhimu kuelekea utekelezaji wa ndoto ya Taifa ya kufikia uchumi wa dola za kimarekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050 kama ilivyoainishwa katika DIRA2050.
 

Akizungumza wakati wa kikao cha kwanza cha uzinduzi wa timu hiyo ya wataalamu, Dkt. Msemwa alisema kuwa timu hiyo inayaoundwa na Watanzania wenye ujuzi mbalimbali imekabidhiwa jukumu la kuandaa Mpango wa kina  wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Mpango huo utaongoza uchumi wa nchi kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia Dira2025 inayoelekea ukingoni.
 

Dkt. Msemwa aliongeza; “Kufanikisha Taifa lenye ustawi, haki, jumuishi na linalojitegemea ndilo lengo kuu kama linavyoainishwa katika DIRA2050, iliyozinduliwa hivi karibuni, ambayo inaenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi yanayoufanya uchumi wa Tanzania kukua na kufikia hadhi ya Taifa lenye kipato cha kati, ngazi ya Juu ifikapo mwaka 2050’. 
 

Hatua hii inakuja wiki mbili tu baada ya Makatibu Wakuu na Naibu wao kukutana Kibaha kujadili kuhusu ukamilishaji wa Mpango wa Marndeleo wa Muda Mrefu (LTPP), ambao utafungua njia ya kuandaliwa kwa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
 

Maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka wa Kwanza wa miaka mitano ni sehemu ya utkelezaji wa DIRA2050, ambayo, pamoja na mambo mengine; ina malengo  makuu manne: Kuwa na Uchumi jumuishi, imara, shirikishi na wenye ushindani; Kujenga Taifa linalohifadhi mazingira na kustahimili mabadiliko ya tabianchi; Kuwa ni nchi yenye kiwango cha juu cha maisha bora na ustawi kwa wote; na Kuwa jamii yenye uwezo wa kidijitali inayothamini ubunifu, huku ikichochea tija na ushindani wa kitaifa.
 

Wiki iliyopita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alikutana na timu hiyo na kuieleza kuwa ana Imani na matumaini makubwa kwao kutokana na uzoefu na uadilifu wao, na kwamba wataweza kuandaa mpango utakaoipeleka Tanzania kwenye nchi ya ahadi ya kufikia uchumi wa thamani ya dola za kimarekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050.