Majukumu yake ni yapi?
Wajibu na majukumu ya Tume ya Taifa ya Mipango ni kama ifuatavyo:-
- Kutathmini hali ya rasilimali za taifa na kuishauri serikali kuhusu matumizi bora ya rasilimali hizo.
- Kuandaa dira ya maendeleo ya taifa, mpango wa maendeleo wa muda mrefu, mpango wa maendeleo wa muda wa kati na mpango wa maendeleo wa muda mfupi, na kusimamia utekelezaji wake.
- Kupendekeza maeneo ya miradi endelevu ya kielelezo na mikakati ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia dira na mikakati ya maendeleo ya Taifa.
- Kufanya tathmini na uchambuzi wa mara kwa mara wa viashiria muhimu vya uchumi ambavyo vinajumuisha urari wa malipo, mtiririko wa fedha na bei, deni la Taifa na kuishauri serikali ipasavyo.
- Kutathmini sera mbalimbali zilizopo kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wake kwa kuzingatia mipango ya maendeleo ya taifa na kupendekeza sera mpya pale inapoonekana inafaa kwa maslahi ya Taifa.
- Kufuatilia utekelezaji wa maeneo muhimu ya vipaumbele vya Taifa kwa sekta mbalimbali za uchumi na kuhakikisha kuwa hatua stahiki zinachukuliwa ili kutatua changamoto zozote za uendeshaji zitakazobainika katika sekta hizo.
- Kutoa mwongozo kuhusu ushirikiano wa kiuchumi kati ya jamhuri ya muungano na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa.
- Kuhakikisha mipango ya sekta inafungamanishwa na mipango ya taifa ili kuwa na matumizi yenye tija ya rasilimali za nchi.
- Kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya kitaifa na miradi ya kielelezo na kuchukua hatua zinazohitajika ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.
- Kuishauri serikali kuhusu mabadiliko yoyote katika mpango wa maendeleo wa taifa ulioidhinishwa.
- Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya baraza la mawaziri kuhusu masuala ya mipango ya maendeleo na usimamizi wa Uchumi.
- Kushauri kuhusu mikakati ya kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini;
- Kukuza mbinu za ubunifu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
- Kutambua na kufanya utafiti kuhusu suala lolote ambalo tume inaona ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
- Kusimamia na kutoa mwongozo katika uandaaji wa mipango mkakati iliyoandaliwa na wizara, idara zinazojitegemea, wakala za serikali, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi nyingine za umma.
- Kuratibu na kuendeleza kada za mipango, uchumi na takwimu na taaluma nyingine zinazofanana na hizo.
- Kuratibu makongamano ya wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili masuala ya mipango ya maendeleo.
- Kubainisha rasilimali za nchi kwa matumizi endelevu kwa maendeleo ya taifa.
- Kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
- Kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na mipango ya maendeleo kadri Rais atakavyoelekeza.