DKT KIDA AKUTANA NA IFAD KUJADILI USHIRIKIANO KATIKA KUFIKIA DIRA 2050 KUPITIA MAGEUZI YA KILIMO
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng, aliyeambatana na Mratibu wa Programu za IFAD nchini, Bi. Jacqueline Machangu-Motcho.
Mazungumzo yao yamelenga kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa vipaumbele vya kitaifa vilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (DIRA 2050) - inayoanza rasmi Julai 1, 2026, na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV).
Maeneo yaliyosisitizwa katika mazungumzo ya viongozi hao ni mageuzi ya sekta ya kilimo, kuimarisha mifumo ya chakula, ajira kwa vijana, na ushiriki wa sekta binafsi ambapo Dkt. Kida ameeleza kuwa Dira 2050 inalenga kuongeza tija, uzalishaji wa kibiashara, na matumizi ya teknolojia.
Aidha alitoa shukrani zake kwa IFAD kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Programu mbalimbali ikiwemo ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) na vilevile alitumia fursa hiyo kumtaarifu mgeni wake kuwa Serikali imekamilisha mfumo mpya wa kitaifa wa kusimamia mipango na miradi ya maendeleo wa e-Delivery System.
Kwa upande wake, Bw. Meng amethibitisha kuwa IFAD itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania kupitia programu za kidijitali za ugani, programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT-YIA), mifumo ya Ubia wa Serikali na Sekta Binafsi (PPP), na kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ili kufikia malengo ya Dira 2050.
#UtekelezajiDira2050
#niJulaiMosi