Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

IDADI YA WATU, AJIRA KUCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI UTEKELEZAJI WA DIRA 2050
11 Sep, 2026
IDADI YA WATU, AJIRA KUCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI UTEKELEZAJI WA DIRA 2050

Dar Es Salaam, Septemba 11, 2026 

Tume ya Taifa ya Mipango imeratibu majadiliano ya Makatibu Wakuu yaliyofanyika leo jijini  Dar es Salaam, yakilenga kutathmini mwenendo wa ongezeko la idadi ya watu, ajira na matumizi, na namna ya kufungamanisha masuala hayo na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Katika majadiliano hayo, imeelezwa kuwa idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 3 kwa mwaka, hali inayomaanisha kuwa idadi ya watu inaweza kuongezeka mara mbili ndani ya takriban miaka 23, huku makadirio ya Dira 2050 yakionesha kuwa idadi ya watu itafikia milioni 118 ndani ya miaka 25 ijayo.

Aidha, imeelezwa kuwa asilimia 54 ya Watanzania wanatarajiwa kuwa vijana, hivyo kuongeza umuhimu wa kutumia rasilimali watu, hususani nguvu kazi ya vijana, kama kichocheo cha shughuli za kiuchumi, uzalishaji na ukuaji wa uchumi.

Vile vile, viongozi hao wamejadili mikakati ya kuhakikisha ongezeko la idadi ya watu linaambatana na upatikanaji wa fursa za kiuchumi, hususani ajira zenye staha, zitakazowezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Miongoni mwa mambo mengine, majadiliano hayo yameangazia umuhimu wa kuimarisha ajira na uzalishaji ili kuongeza uwezo wa wananchi kushiriki katika uchumi, sambamba na kuchochea matumizi na ukuaji wa uchumi katika utekelezaji wa Dira 2050.