TUME YA TAIFA YA MIPANGO YATAFUTA MBADALA WAKUTATUA SOKO LA AJIRA KWA VIJANA
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Mbaga Kida, amefanya mazungumzo yaliyolenga kukuza fursa za ajira na mabadiliko ya kiuchumi nchini alipokutana na ujumbe wa wataalamu wa uchumi wa kimataifa.
Ujumbe huo, umehusisha Prof. Dirk Willem te Velde, Mtafiti Mkuu Mwandamizi na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uchumi wa Kimataifa kutoka taasisi ya ODI, pamoja na Dkt. Louise Fox, Mchumi kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Katika mazungumzo hayo, pande zote zimejadili mabadiliko ya kiuchumi na ajira kupitia mipango ya pamoja, kwa kubaini mbinu za kuongeza tija katika sekta zinazozalisha ajira kwa wingi ili ukuaji wa uchumi uwe na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Aidha, wamezungumzia kuimarisha ushirikiano wa kitafiti na kisera, ukilenga kutumia matokeo ya tafiti za kiuchumi kutoka ODI na USAID katika kuandaa sera zitakazochochea soko la ajira kwa vijana.
Mazungumzo hayo, yanakuja wakati Tume ya Taifa ya Mipango ikiendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya maendeleo ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaenda sambamba na utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa ajira.