IPU YAHITIMISHWA ARUSHA
Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) umehitimishwa leo Oktoba 9, 2026, jijini Arusha huku ‘Banda la Karibu Tanzania’ likitoa fursa kwa wageni wa kimataifa kufahamu historia, mafanikio na vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania.
Katika kipindi chote cha siku tano za mkutano huo, banda lilipokea wageni zaidi ya 150 kwa siku, wakiwemo Maspika zaidi ya 10, Mawaziri na Wabunge kutoka nchi mbalimbali wanachama wa IPU.
Wageni hao, walipata maelezo kuhusu historia ya Tanzania; Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mchango wa nchi katika harakati za ukombozi wa Afrika, pamoja na juhudi zake za kudumisha amani na usalama katika bara la Afrika na Duniani.
Aidha, wageni hao walielezwa hatua zilizopigwa katika kuboresha huduma za kijamii ikiwemo upatikanaji wa maji na umeme; huduma za afya, kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuimarisha usawa wa kijinsia.
Pia, walifahamishwa kuhusu miradi ya kimkakati na mchango wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa ujumla, ushiriki wa Tume ya Taifa ya Mipango kupitia banda hilo umechangia kuitangaza Tanzania kwa jumuiya ya kimataifa, kwa kuonesha mwelekeo wa maendeleo ya nchi na vipaumbele vyake, hususan Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalo jitegemea.