TUME YA TAIFA YA MIPANGO NA TASAF WAKUTANA KUJADILI PROGRAMU ZA KUPUNGUZA UMASKINI
TUME YA TAIFA YA MIPANGO NA TASAF WAKUTANA KUJADILI PROGRAMU ZA KUPUNGUZA UMASKINI
Tume ya Taifa ya Mipango imefanya kikao na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali iliyopo na inayotarajiwa katika kupunguza umaskini nchini kwa kuzingatia malengo ya Dira 2050.
Akiongoza kikao hicho leo jijini Dodoma, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia Mipango ya Kitaifa Dkt. Mursali Milanzi amesema kuwa Tume kwa kushirikiana na TASAF watakuwa na mikakati mahsusi wakishirikisha taasisi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) ili kuwa na mwelekeo mmoja katika kupunguza umaskini nchini.
Dkt Milanzi ameeleza kuwa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Tano (FYDP IV: 2026/27 – 2030/31) unalenga kupunguza kiwango cha umaskini uliokithiri kutoka asilimia 8 hadi 5 ifikapo mwaka 2030/31. Hivyo Tume inawajibu wa kuratibu wadau wote wanaotekeleza afua mbalimbali za kupunguza umaskini ili kujua endapo utekelezaji wake unalenga shabaha zilizowekwa katika mipango ya kitaifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray amesema kuwa mfuko huo utaendelea kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango kwa kuboresha shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kupitia mfuko huo ili kuhakikisha malengo yake yanaendana na malengo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Tano.
Kikao hicho pamoja na mambo mengine pia kimekubaliana kuandaa mwongozo wa pamoja ambao utatoa mwelekeo wa uratibu na ufuatiliaji wa programme za kupunguza umaskini zinazotelekezwa nchini.
#TekelezaDira2050