Katibu Mkuu Kiongozi awaambia Makatibu Wakuu katika kikao kazi: DIRA 2050 siyo kazi za mazoea

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Dkt. Moses Kusiluka, amefungua kikao kazi cha siku mbili kwa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wote kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa DIRA 2050, siku chache tu baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 17 Julai 2025.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyewakilishwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw. Onorius Njole, Wajumbe wa Kikosi Kazi cha kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP) wakiongozwa na Balozi, Dkt. Asha-Rose Migiro, baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, pamoja na watumishi na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Mipango (NPC).
Dkt. Kusiluka, aliyefungua kikao hicho jana (04.08.2025) katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha, aliwataka washiriki kufaham kikamilifu na kuelewa DIRA 2050, pamoja na maudhui ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP).
Aliwahimiza washiriki wote kuchangia kwa dhati ili kuandaa LTPP inayotekelezeka na halisia, huku akisisitiza kuwa huu si wakati wa kuendelea na kazi kwa mazoea kwani kupitia LTPP hiyo, Tanzania inatarajiwa kufikia malengo ya DIRA 2050 ikiwemo kuwa na Pato la Taifa (GDP) la dola trilioni moja za Kimarekani ifikapo mwaka 2050.
Alisisitiza kuwa Makatibu Wakuu wanapaswa kutoa mchango mpana usioishia tu katika wizara zao, bali kwa maslahi ya Taifa zima, kwa kuwa huwa wanabadilishana wizara mara kwa mara.
Katika hotuba yake ya ukaribisho, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida alimshukuru Katibu Mkuu Kiongozi kwa kuchukua muda wake kushiriki kikao hicho muhimu kwa utekelezaji wa DIRA 2050 katika kupitia maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa miaka 25, Muda wa kati na mfupi ya miaka mitano na mmoja, mtawalia.
Akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa DIRA 2050, Katibu Mtendaji wa NPC, Dkt. Fred Msemwa aliwakumbusha maagizo yaliyotolewa na Rais, Dkt. Samia wakati wa uzinduzi wa DIRA 2050 tarehe 17 Julai 2025 kuwa yazingatiwe kikamilifu wakati wa utekelezaji.
Dkt. Msemwa alizitaja maagizo hayo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya mtazamo katika utendaji kazi, kila wizara kufanya uhakiki wa sera zilizopo kama zinaendana na DIRA 2050, kufanyia marekebisho sheria ili ziendane na DIRA 2050, kushirikisha sekta binafsi kama mhimili mkuu, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kuendesha kampeni ya uelimishaji wa umma ili kila Mtanzania aelewe maudhui ya DIRA 2050.
Kikao kazi hiki kimeandaliwa na NPC, kama sehemu ya hatua za awali za utekelezaji wa DIRA 2050 kwa lengo la kupata maoni ya Makatibu Wakuu katika uandaaji wa Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa miaka 25, na mipango ya kati na mfupi ya miaka mitano na mwaka mmoja, mtawalia.