KITILA MKUMBO: DIRA 2050 INAHITAJI UTEKELEZAJI WENYE MATOKEO YANAYOPIMIKA
KITILA MKUMBO: DIRA 2050 INAHITAJI UTEKELEZAJI WENYE MATOKEO YANAYOPIMIKA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb), amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji ushirikiano wa wadau wote, mifumo madhubuti ya uwajibikaji na matumizi yenye tija ya rasilimali ili kufikia malengo ya maendeleo ya nchi.
Prof. Kitila ameyasema hayo akiwasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2025/26, utekelezaji wa robo ya kwanza ya mwaka 2026/27, pamoja na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2027/28. Leo tarehe 23 Oktoba, 2050.
Amesema taarifa hizo ni muhimu katika kutathmini hatua zilizopigwa na kuweka msingi wa utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV), wa mwaka 2026/27–2030/31, ambao ni wa kwanza katika utekelezaji wa Dira 2050.
Akifafanua umuhimu wa taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka 2026/27, Prof. Kitila amesema ni hatua ya mwanzo katika kutafsiri malengo ya Dira 2050 kuwa programu, majukumu ya taasisi na matokeo yanayoweza kupimika, huku ikiweka msingi wa uwajibikaji katika safari ya maendeleo ya taifa ya miaka 25 ijayo.
“Dira 2050 si waraka mwingine wa Serikali tu. Ni dhamira yetu ya kitaifa ya kuubadilisha uchumi wa Tanzania, kuimarisha uwezo wa wananchi, kuboresha maisha yao na kuhakikisha kwamba tunajenga ustawi kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” amesema.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa Dira 2050 si jukumu la Serikali pekee, bali unahitaji ushiriki wa Bunge, sekta binafsi, mamlaka za Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, taasisi za elimu ya juu na utafiti, asasi za kiraia, washirika wa maendeleo, Watanzania wanaoishi nje ya nchi na wananchi wote.
Amesisitiza kuwa kipaumbele cha Serikali ni kuhamisha Dira kutoka kwenye matarajio na mipango kwenda kwenye utekelezaji wenye tija na matokeo yanayopimika, yatakayochangia kufikia ustawi wa pamoja na maendeleo endelevu ya Tanzania.