Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

Utekelelezaji wa DIRA 2050 waanza kwa kasi: Toleo la kwanza la Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano kukamilika Novemba 2025
05 Aug, 2025
Utekelelezaji wa DIRA 2050 waanza kwa kasi: Toleo la kwanza la Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano kukamilika Novemba 2025

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dkt. Fred Msemwa, amemjulisha Katibu Mkuu Kiongozi (CS), Balozi, Dkt. Moses Kusiluka kuwa Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati (miaka mitano ya mwanzo) unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba mwaka huu.

Hayo yalibainishwa na Dkt. Msemwa alipokuwa akitoa muhtasari wa kikao kazi cha siku mbili kilichowakutanisha Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wote kwa ajili ya kufanya mapitio ya Mpango wa Maendeleo wa Mtazamo wa Muda Mrefu (LTPP), kilichofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha.

Kwa mujibu wa Dkt. Msemwa, mapitio ya LTPP yalihusisha makundi matano ambayo yalijadili kwa kina kuhusu mpango uliohusosha kufanya mapitio ya sera mbalimbali pamoja na sheria ili kuweka mazingira rafiki ya utekelezaji wa LTPP.

Alisema kuwa baad ya mapitio hayo, kazi inayofuata kwa NPC ni kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano,  ambao unatarajiwa kuwa tayari mwezi Novemba kwa ajili ya mapitio na mashauriano kutoka kwa wadau muhimu.

Katika hotuba yake ya kufunga kikao hicho, Katibu Mkuu Kiongozi alielekeza Makatibu Wakuu wote kurudi na kueneza elimu kuhusu maudhui ya DIRA 2050 ili kila Mtumishi wa Umma katika ngazi ya wizara aweze kuifahamu vizuri DIRA hiyo. Aliongeza kuwa muhtasari wote ulioelezwa na Dr. Msemwa utachukuliwa na ofisi yake kwa ajili ya ufuatiliaji makini na utekelezaji mzuri.

Alisisitiza: “Ninayachukua yote yaliyozungumzwa na Dkt. Msemwa ili yawe rahisi kufuatiliwa na kusimamiwa; na yasichukuliwe kama ni maelekezo kutoka taasisi ya Tume ya Mipango tu, bali yachukuliwe kama ni hitaji la pamoja kwa wote.” 

Pia aliagiza kuwa sera zote zinapaswa kuwa zimepitiwa ili kulingana DIRA 2050 kabla ya kuanza kutekelezwa kwa Dira hiyo Julai 2026.

Akizungumzia kuhusu Utumishi wa  Umma katika kuendana na DIRA 2050, Katibu Mkuu Kiongozi alisema, Serikali itaendelea kuboresha Utumishi wa  Umma ili kuwepo na watumishi bora na wa kiwango cha juu kwa ajili ya kuendana na mwelekeo wa DIRA 2050.