Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango (NPC)

RAIS SAMIA AZINDUA DIRA 2050, ATOA MAELEKEZO MAZITO KUHUSU UTEKELEZAJI NA UWAJIBIKAJI
21 Jul, 2025
RAIS SAMIA AZINDUA DIRA 2050, ATOA MAELEKEZO MAZITO KUHUSU UTEKELEZAJI NA UWAJIBIKAJI

RAIS SAMIA AZINDUA DIRA 2050, ATOA MAELEKEZO MAZITO KUHUSU UTEKELEZAJI NA UWAJIBIKAJI

Dodoma, Julai 17, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amezindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kusisitiza dhamira ya Serikali kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa uwazi, umakini na matokeo yenye tija kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma, Mhe. Rais Samia amesema kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha mfumo wa uwajibikaji na upimaji wa matokeo katika taasisi zote za umma ili kuhakikisha Dira hiyo inatekelezwa kwa mafanikio makubwa.

“Utekelezaji wa Dira 2050 hautakuwa na maana endapo hautafuatiliwa kwa uwazi, umakini na ufanisi. Tutapima kwa matokeo, si kwa maelezo. Ni lazima kila hatua tuone faida yake kwa wananchi,” alisisitiza Rais Samia.

Akiweka mkazo katika suala la ufuatiliaji, Mhe. Rais Samia ameielekeza Tume ya Taifa ya Mipango, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kuandaa haraka mfumo wa kitaasisi wa ufuatiliaji na tathmini utakaoainisha wazi majukumu, muda wa utekelezaji na vigezo vya kupima mafanikio katika kila hatua ya utekelezaji wa Dira.

“Kila taasisi ya Serikali italazimika kuwa na vigezo vya kupima utendaji (Key Performance Indicators – KPIs) vinavyoendana na malengo na shabaha ya Dira,” alisema.

Aidha, Rais Samia ameelekeza Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza mapitio ya sheria na sera zote zinazoweza kuwa kikwazo katika utekelezaji wa Dira hiyo, ili ziboreshwe na kuendana na mwelekeo mpya wa Taifa.

Katika kuimarisha ushirikiano na mshikamano wa kitaifa, Mhe. Rais ametoa wito kwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, sekta binafsi, asasi za kiraia, taasisi za dini na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira 2050. Aidha, amezitaka taasisi zote za umma na binafsi kuanza mapema maandalizi ya kutekeleza majukumu yao ifikapo Julai 2026.

Kwa kaulimbiu ya “Tanzania Tuitakayo”, Rais Samia amesema ni wakati wa kuachana na mazoea na kuingia katika awamu mpya ya upangaji na utekelezaji wa maendeleo kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu.

“Things cannot be business as usual. Lazima tubadilishe namna tunavyofanya kazi,” amehitimisha.