Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

SERIKALI KUIMARISHA UFUATILIAJI WA MALENGO YA DIRA 2050 KUPITIA MFUMO WA E-DELIVERY – DKT. PIUS CHAYA
04 Nov, 2026
SERIKALI KUIMARISHA UFUATILIAJI WA MALENGO YA DIRA 2050 KUPITIA MFUMO WA E-DELIVERY – DKT. PIUS CHAYA

SERIKALI KUIMARISHA UFUATILIAJI WA MALENGO YA DIRA 2050 KUPITIA MFUMO WA E-DELIVERY – DKT. PIUS CHAYA

Serikali imeanzisha Mfumo wa e-Delivery kwa lengo la kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo nchini, ili kuhakikisha matokeo yake yanachangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yamesemwa leo, tarehe 27 Oktoba 2026, na Dkt. Pius Chaya, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, akijibu swali la Mbunge wa Magomeni, Mheshimiwa Imamu Mtumwa Vuai, kuhusu namna Serikali itakavyohakikisha Mfumo wa e-Delivery unawezesha Bunge na wananchi kupima utekelezaji wa malengo ya Dira 2050.

Dkt. Chaya ameeleza kuwa mfumo huo umeunganisha mipango ya muda mrefu, wa kati na mfupi, ikiwemo Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/27–2050/51, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), mipango ya kisekta na kikanda, pamoja na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya mwaka 2030 na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063, hatua inayowezesha utekelezaji wa mipango hiyo kufuatiliwa kwa kuzingatia vipaumbele na malengo ya maendeleo ya Taifa.

Aidha, Dkt. Chaya amesema Serikali imetoa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo kwa watumishi takribani 940 kutoka wizara, taasisi, mikoa na halmashauri nchini. Am ezitaka taasisi zote za umma kutumia mfumo wa e-Delivery katika hatua zote za usimamizi wa miradi, kuanzia uibuaji, uandaaji na uidhinishaji hadi ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa wakati. Amesisitiza kuwa miradi yote ya maendeleo inayoendelea inapaswa kusajiliwa katika mfumo huo ili kurahisisha ufuatiliaji wa maendeleo yake na kupima mchango wake katika kufikia malengo ya Dira 2050. 

Kupitia dashibodi za mfumo huo, Bunge na wananchi wataweza kupata taarifa za utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo, hivyo kuimarisha uwazi, uwajibikaji na uwezo wa kupima matokeo ya juhudi za Serikali katika kutekeleza Dira 2050.