Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

TANZANIA, ABSA GROUP ZAJADILI UWEKEZAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA Dira 2050
04 Nov, 2026
TANZANIA, ABSA GROUP ZAJADILI UWEKEZAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA Dira 2050

TANZANIA, ABSA GROUP ZAJADILI UWEKEZAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA Dira 2050

Serikali ya Tanzania na Absa Group zimejadili fursa za uwekezaji na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta za kipaumbele zilizoainishwa katika Dira 2050.

Mazungumzo hayo yamefanyika  leo Oktoba 14, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, yakilenga kuimarisha ushirikiano katika kufanikisha miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb.) aliyeambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Mipango) na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi M. Kida.

Dkt. Mwamba amesisitiza haja ya kupanua upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kuimarisha mifumo ya ufadhili wa miradi ya maendeleo na kuwezesha mashirika ya umma pamoja na sekta binafsi kupata fedha zinazokidhi mahitaji na uwezo wao wa kifedha. Hatua hiyo inalenga kuongeza uwekezaji, uzalishaji na ushindani wa uchumi.

Kwa upande wake, Dkt. Kida amesema mazungumzo hayo yanafungua fursa za ushirikiano katika kufadhili uwekezaji wa kimkakati, hususan miundombinu na sekta zinazozalisha thamani na ajira, sambamba na kuimarisha biashara ya kikanda.

Ujumbe wa Absa Group, ulioongozwa na Sola Adegbesan, Meneja Mtendaji wa Huduma za Biashara na Uwekezaji katika Kanda za Afrika, ulionesha kuvutiwa na miradi ya kimkakati ya Tanzania, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), nishati na bandari, ambayo ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji na kukuza biashara ya kikanda.