TANZANIA TUITAKAYO 2050 INAANZA NA UELEWA WA PAMOJA
TANZANIA TUITAKAYO 2050 INAANZA NA UELEWA WA PAMOJA
Tume ya Taifa ya Mipango imewakutanisha wanahabari katika mafunzo maalumu kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa lengo la kuwajengea uwezo na ufahamu wa kina kuhusu mipango ya kitaifa ya maendeleo hususani Dira 2050.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Dkt. Tausi M. Kida, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, ambaye amesisitiza umuhimu wa wanahabari kuwa daraja la uelewa kuelekea ustawi wa pamoja.
“Mafunzo haya yanatarajiwa kuwawezesha kutafsiri Dira 2050, Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/27-2050/51 (LTPP), na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/27-2030/31(FYDP) ili muweze kutoa ufafanuzi sahihi kwa jamii” amesema Dkt. Kida.
Aidha, ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuwakumbusha wananchi mahali ambapo Taifa limetoka, lilipo na linakoelekea.
Kwa upande wake, Mweneyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Bw. Deodatus Balile ameishukuru Tume ya Taifa ya Mipango kwa kuendelea kuwashirikisha wanahabari katika mchakato mzima wa maandalizi na hatua za utekelezaji wa Dira, akitoa wito wa waandishi wa habari kuongeza ubunifu katika kuwasilisha habari za Dira 2050.