Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

TANZANIA YAANZA SAFARI YA UCHUMI WA DOLA TRILIONI 1 IFIKAPO 2050
06 Aug, 2026
TANZANIA YAANZA SAFARI YA UCHUMI WA DOLA TRILIONI 1 IFIKAPO 2050

Katika Jukwaa la Ngazi ya Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa la Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu lililofanyika New York, Dkt. Tausi Kida (Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango) ameeleza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV), ikiwa ni hatua ya kwanza ya kutekeleza Dira 2050 iliyozinduliwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Julai 17, 2025.


Dkt. Kida amesema kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026. Aidha, kilimo, misitu na uvuvi vilichangia asilimia 24.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025 na kuendelea kuajiri zaidi ya nusu ya Watanzania.


Mafanikio makubwa yametajwa pia kupitia ushirikiano na UNCDF, yakihusisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ambao umeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025.


Tanzania pia imekuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutoa hatifungani ya kijani katika ngazi ya mamlaka za serikali za mitaa, iliyokusanya dola za Marekani milioni 20.8 kwa ajili ya miundombinu ya maji safi.


Mafanikio hayo yalitajwa na Ofisa Mkuu wa Fedha wa UNCDF, Bw. Karen Vardanyan, katika kikao cha pembezoni mwa Jukwaa la Ngazi ya Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa la Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.


Katika kikao hicho pia, Tanzania iliwakaribisha wadau kushiriki katika uwasilishaji wa Mapitio ya Tatu Hiari ya Nchi ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, utakaofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo, tarehe 14 Julai 2026.