TANZANIA YAONESHA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA SDGS UMOJA WA MATAIFA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo leo amewasilisha Taarifa ya Tatu ya Nchi ya Hiari ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika Jukwaa la Ngazi ya Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa linalosimamia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (High-Level Political Forum HLPF) linaloendelea na Mkutano wake Jijini New York, Marekani.
Katika wasilisho hilo Mhe. Waziri ameweka wazi baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kufuatia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika utekelezaji wa malengo hayo ikihusisha Upatikanaji wa maji safi vijijini ulioongezeka kutoka 72.3% mwaka 2020 hadi 85.3% mwaka 2025.
Mafanikio mengine yamehusu nishati, ambapo wananchi wenye huduma ya umeme wameongezeka kufikia asilimia 86.2, huku uwezo wa kuzalisha umeme nao ukiongezeka zaidi ya mara mbili.
Vile vile, taarifa hiyo inaonesha kuwa Tanzania imefanya vizuri katika lengo namba 9, viwanda na miundombinu iliyochangia kuongezeka kwa idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa Tren ambao wameongezeka kutoka milioni 1.2 hadi milioni 4.1.
Kuhusu lengo la 17 ushirikiano kwa maendeleo, Mhe. Waziri amesema kuwa utekelezaji wa malengo hayo unafanyika kwa ushirikiano mkubwa bainfa ya wadau wote, ikiwemo sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo.
“Zaidi ya mashirika 824 ya kiraia na taasisi 1,000 za sekta binafsi zilishiriki katika maandalizi ya taarifa hii” alieleza.
Mhe. Prof. Mkumbo, alieleza maeneo saba ya kipaumbele yatakayoharakisha utekelezaji wa SDGs kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV).
Kwa ujumla, Tanzania imeonesha si tu mafanikio yaliyofikiwa, bali pia dhamira ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ajenda ya 2030 katika miaka minne iliyosalia.