Tume ya Mipango Yaadhimisha Wiki ya Siku ya Mwanamke Duniani kwa Kutoa Msaada Gereza la Isanga

Katika kuadhimisha Wiki ya Siku ya Mwanamke Duniani, watumishi wa Tume ya Taifa ya Mipango wametembelea Gereza la Isanga jijini Dodoma na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wafungwa wa kike na wa kiume. Zoezi hilo, limefanyika Machi 5, 2025, ni ishara ya kuonesha ukarimu aliyo nao Mwanamke wa Kitanzania na kuhamasisha mshikamano wa kijamii kwa kuzingatia utu na haki za binadamu.
Msaada uliotolewa unajumuisha viatu (crocks), mafuta ya kujipaka na kupikia, sabuni, nguo, na mahitaji mengine muhimu. Watumishi wa Tume wamesema hatua hiyo ni sehemu ya mchango wao kwa jamii, wakisisitiza umuhimu wa kuwajali na kuwapa matumaini wafungwa. Maadhimisho rasmi ya Siku ya Mwanamke Duniani nchini Tanzania yanatarajiwa kufanyika Machi 8, 2025, jijini Arusha.