Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

TUME YA TAIFA YA MIPANGO, MAHAKAMA ZAKUTANA KUJADILI HAKI KATIKA DIRA 2050
04 Nov, 2026
TUME YA TAIFA YA MIPANGO, MAHAKAMA ZAKUTANA KUJADILI HAKI KATIKA DIRA 2050

TUME YA TAIFA YA MIPANGO, MAHAKAMA ZAKUTANA KUJADILI HAKI KATIKA DIRA 2050

Dodoma. 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi M. Kida, amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John A. Jingu, Pamoja na Msajili wa Mahakama Bi. Eva Nkya kuhusu nafasi ya haki katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mazungumzo hayo yalijikita katika namna masuala ya haki, utawala bora, usawa wa fursa na uimarishaji wa taasisi yanavyoweza kuzingatiwa katika safari ya maendeleo ya Tanzania.

Dkt. Kida ameleza kuwa, Dira 2050 imeweka demokrasia, haki na uhuru miongoni mwa misingi muhimu ya maendeleo katika ujenzi wa Taifa jumuishi, lenye ustawi, haki na linalojitegemea. 

“Msingi huu unakusudia kuhakikisha kila mtu anafurahia uhuru, ulinzi wa maisha yake na haki zote za msingi zilizowekwa kikatiba, chini ya mahakama zilizo huru, hivyo Dira inasisitiza utawala wa sheria, ulinzi wa haki za msingi, usawa wa fursa na uwepo wa taasisi imara zinazotoa huduma kwa uadilifu na bila upendeleo” ameeleza Dkt. Kida. 

Aidha, aligusia umuhimu wa kuhakikisha dhana ya haki iliyoainishwa katika Dira 2050 inatafsiriwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo, ikiwemo upatikanaji wa huduma bora, usawa wa fursa na matumizi yenye tija ya rasilimali za Taifa.

Kwa upande wake, Dkt. Jingu alisema ni jambo jema kwa Tume ya Taifa ya Mipango na Mahakama kukutana na kujadili masuala hayo, akisisitiza kuwa kuna kila sababu kwa taasisi hizo kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha haki na utawala wa sheria vinaendelea kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira 2050, sambamba na kujenga taasisi imara zinazowajibika na zinazolinda maslahi ya wananchi.

Kwa ujumla, mazungumzo hayo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano wa taasisi katika kutafsiri Dira 2050 kuwa matokeo yanayogusa maisha ya wananchi, kwa kuhakikisha maendeleo yanaenda sambamba na haki, usawa na uwajibikaji.