Tume ya Taifa ya Mipango na UNFPA Wajadili Ushirikiano wa Kimkakati na Masuala ya Idadi ya Watu katika Mipango ya Maendeleo

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, pamoja na Dkt. Mursali Milanzi, Naibu Katibu Mtendaji – Mipango ya Kitaifa, leo tarehe 2 Julai 2025 jijini Dar es Salaam, wamekutana na kufanya kikao na Mark Bryan Schreiner, ambaye ndiye Mwakilishi wa UNFPA nchini Tanzania, pamoja na wawakilishi wengine kutoka Shirika hilo kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya kimkakati.
Katika kikao hicho, UNFPA imetoa pongezi kwa Dkt. Msemwa kufuatia uteuzi wake hivi karibuni, pamoja na kuchambua maeneo ya ushirikiano yanayoendelea na yale yajayo, vile vile wamejadili masuala muhimu yanayohusiana na idadi ya watu na maendeleo, hususan namna ya kuingiza tafsiri ya takwimu za kidemografia katika mipango ya kitaifa. UNFPA imethibitisha upya dhamira yake ya kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika kutekeleza vipaumbele vyake vya maendeleo kupitia msaada wa kitaalamu na kifedha.