Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

TUME YA TAIFA YA MIPANGO YAHAMASISHA UTEKELEZAJI DIRA 2050 KWENYE MAONESHO YA SABA SABA ‎ ‎
06 Aug, 2026
TUME YA TAIFA YA MIPANGO YAHAMASISHA UTEKELEZAJI DIRA 2050 KWENYE MAONESHO YA SABA SABA ‎ ‎

Tume ya Taifa ya Mipango imeshiriki Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kwa kutoa elimu kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na nafasi yake katika kuendeleza biashara na uwekezaji. ‎

 Akizungumza katika maonesho hayo, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia Biashara na Ubunifu, Dkt. Blandina Kilama, amesema kuwa Tume haiishii katika kuandaa mipango ya maendeleo pekee, bali pia inahakikisha ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ili biashara, uwekezaji na ubunifu viwe chachu ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. ‎ ‎

Amesema Dira 2050 inaweka msisitizo katika kujenga uchumi shindani unaoongozwa na sekta binafsi, ukichochewa na viwanda, teknolojia, ubunifu na biashara yenye ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa hivyo ushiriki wa Tume katika maonesho hayo unalenga kuwajengea wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi uelewa wa nafasi yao katika kufanikisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kipato cha juu, jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2050. ‎ ‎

Mbali na kuwepo katika banda la Tume ya Taifa ya Mipango Dkt Blandina pia ametembelea mabanda ya wizara na taasisi mbalimbali katika kuhamasisha watendaji juu ya utekelezaji wa Dira 2050 pamoja na vipaumbele vyake. ‎