TUME YA TAIFA YA MIPANGO YAKAMILISHA MAFUNZO YA MWONGOZO WA NDPAG KWA WATENDAJI 500
Tume ya Taifa ya Mipango imekamilisha utoaji wa mafunzo ya Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo (NDPAG) Kwa Maafisa Mipango na Wakuu wa Idara/Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathimini 500 kutoka nchini nzima
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Meneja Miradi ya kitaifa kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Bw. Royal John Lyanga, amesema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo maafisa hao ili waondokane na kufanya kazi kwa mazoea kuelekea Julai Mosi ambapo utekelezaji wa Dira 2050 utaanza rasmi.
Ameeleza kuwa Miradi yote ya kitaifa kwenye mikoa, wilaya na halmashauri kuanzia sasa itaandaliwa kitaalamu kwa kufuata mwongozo huo na kuwasilishwa kwenye ngazi husika kupitia mfumo wa e-Delivery.
Mfumo wa e-Delivery utazingatia viwango vya ubora wa maandiko ya miradi, mfumo mzima wa ufuatiliaji na tathimini pamoja na maandalizi bora ya miradi.
Tume ya Taifa ya Mipango imeendelea kutoa mafunzo Kwa watendaji wa kada mbalimbali nchini kwa lengo la kujenga uelewa wa miongozo na mifumo mbalimbali itakayotumika kuanzia Julai Mosi katika utekelezaji wa Dira 2050.