Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

TUME YA TAIFA YA MIPANGO YAKUSANYA TAARIFA ZA PROGRAMU ZA KIELELEZO NA MIRADI SHIKIZI
04 Nov, 2026
TUME YA TAIFA YA MIPANGO YAKUSANYA TAARIFA ZA PROGRAMU ZA KIELELEZO NA MIRADI SHIKIZI

TUME YA TAIFA YA MIPANGO YAKUSANYA TAARIFA ZA PROGRAMU ZA KIELELEZO NA MIRADI SHIKIZI 

Tume ya Taifa ya Mipango kwa kushirikiana na wizara za kisekta na taasisi za umma inaendelea na zoezi la kukusanya taarifa (fact-findings) za programu za kielelezo na miradi shikizi nchi nzima kwa lengo la kupata taarifa za kina na sahihi za programu hizo. 

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Bw. Royal Lyanga ambaye ni Mkurugenzi anayesimamia Maeneo Muhimu yenye Matokeo Makubwa kwa Taifa kutoka Tume ya Taifa ya Mipango amesema lengo la zeozi hilo ni kuhakikisha kuna ufanisi katika utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) 2026/27 – 2030/31.

Bw. Lyanga amesema kuwa taarifa zinazokusanywa ni muhimu kwa kuwa zitasaidia kuhakikisha kuwa programu saba za kielelezo zilizobainishwa zinatekelezwa kwa kuzingatia malengo makubwa ya Dira 2050. 

Aidha, ameeleza kuwa mbali na programu hizo za kielelezo, Tume ya Taifa ya Mipango inakusanya taarifa za miradi yote ya kimkakati ambayo ina mchango chanya katika kufikia matokeo makubwa kwa nchi, ikijumuisha miradi ya Barabara, nishati, maji, miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, miradi ya mifumo ya teknolojia ya mawasiliano pamoja na miradi mingine ya kisekta. 

Aidha Bw. Lyanga amefafanua kuwa baada ya kukusanya taarifa hizo, miradi yote itaingizwa katika maabara (Labs) kwa kuwashirikisha wadau wote wa sekta kwenye kila mradi wa kielelezo ambapo itasaidia kupata matokeo chanya kwa kutatua changamoto mbalimbali ambazo zitabainika kwa kila mradi, kufungamanisha miradi hiyo na sekta nyingine, kuimarisha wigo wa ushirikishwaji wa sekta binafsi na kutambua uhalisia wa miradi hiyo kwa kuzingatia malengo ya Dira 2050 hususan katika kuzalisha ajira kwa vijana, kuboresha maisha ya watu na kuongeza mapato ya Serikali.