TUME YA TAIFA YA MIPANGO YATETA NA SEKTA BINAFSI KUHUSU MWONGOZO WA USHIRIKISHWAJI
Tume ya Taifa ya Mipango imeandaa Mwongozo na Mkakati wa Kitaifa wa ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa ikiwemo Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) katika utekelezaji wa Dira 2050 inayoanza rasmi Julai Mosi 2026
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango Dkt Tausi Kida wakati akifungua warsha iliyowakutanisha wadau wa sekta binafsi pamoja na Tume, kujadili na kuboresha Mwongozo na Mkakati huo ambao utaimarisha uratibu na ushirikiano, na kukuza mazingira wezeshi yatakayosaidia kukuza uvumbuzi, na ukuaji endelevu wa uchumi.
Dkt Kida amebainisha kuwa mwongozo na mkakati huo ni miongoni mwa juhudi za Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi ili kufikia lengo la sekta hiyo kuchangia asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira 2050 pamoja na kuchochea uwekezaji, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika sekta za kipaumbele, na uratibu wa sera unaotabirika zaidi.
Kadhalika Dkt Kida amewahakikishia wadau hao wa sekta binafsi kuwa Tume ya Taifa ya Mipango imejipanga kutumia mwongozo na mkakati huo kama chombo cha kutekeleza ushirikishwaji wa sekta binafsi katika mzunguko mzima wa mipango ya maendeleo, kuanzia utambuzi wa mradi, utekelezaji, ufuatiliaji hadi tathmini.
#UtekelezajiDira2050
#niJulaiMosi