UCHUMI WAKUA, KILIMO NA UJENZI VIKISHIKA KASI
Hali ya uchumi wa Taifa imeendelea kuimarika, ambapo wastani wa Pato la Taifa kwa kila Mtanzania uliongezeka kwa asilimia 7.4 na kufikia shilingi 3,544,124 (dola 1,390) mwaka 2025, kutoka shilingi 3,299,637 (dola 1,264) iliyorekodiwa mwaka 2024.
Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Mhe. Prof. Kitila A. Mkumbo, wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027.
Sekta Zinazobeba Uchumi wa Nchi
Taarifa ya Hali ya Uchumi inaonesha kuwa sekta ya kilimo imeendelea kuwa utosini kama muhimili mkuu wa uchumi wa nchi kwa kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa. Hapa ndipo nguvu ya uchumi ilipotoka:
• Kilimo: Kimechangia 24.3% ya Pato Ghafi la Taifa.
• Ujenzi: Umechangia 11.9%.
• Uchimbaji Madini na Mawe: Umechangia 10.3%.
• Biashara na Matengenezo: Imechangia 8.6%.
• Usafirishaji na Uhifadhi Mizigo: Umechangia 8.3%.
Sekta Zilizokua kwa Kasi Zaidi
Wakati kilimo kikichangia kiasi katika Uchumi, Mhe. Prof. Mkumbo amesema sekta za fedha na bima (ndizo zilizokimbia kwa kasi kubwa zaidi ya ukuaji, zikifuatwa na shughuli za uzalishaji na usambazaji umeme na gesi.
Orodha ya sekta zilizokua kwa kasi:
• Fedha na Bima: 15.7%
• Umeme na Gesi: 11.8%
• Uchimbaji Madini na Mawe: 9.4%
• Habari na Mawasiliano: 8.8%
• Sanaa na Burudani: 8.5%
• Usafirishaji na Uhifadhi Mizigo: 8.0%
Mfumuko wa Bei: Bei za Vyakula Zapanda Kidogo
Kuhusu hali ya maisha na bei za bidhaa sokoni, Mhe.Prof. Mkumbo ameeleza kuwa mfumuko wa bei uliongezeka kidogo hadi kufikia wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 3.1 ya mwaka 2024. Ongezeko hili limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei za vyakula.
Hata hivyo, Prof. Mkumbo amewatoa hofu wananchi kwa kueleza kuwa ongezeko hilo bado ni salama kwani lipo ndani ya lengo la nchi (asilimia 3.0 hadi 5.0)