Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

UTEKELEZAJI DIRA 2050: MIRADI 150 YA MAENDELEO YASAJILIWA KWENYE MFUMO WA e- DELIVERY
05 Sep, 2026
UTEKELEZAJI DIRA 2050: MIRADI 150 YA MAENDELEO YASAJILIWA KWENYE MFUMO WA e- DELIVERY

Tume ya Taifa ya Mipango imetoa wito kwa Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka wizara na taasisi mbalimbali kuongeza kasi ya kusajili miradi  kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Mipango na Miradi ya Maendeleo wa e -Delivery ili kuharakisha utekelezaji wa Dira 2050

Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia Menejimenti ya Utendaji na Tathmini  Bw. Sosthenes Kewe alipofungua  kikao kazi cha tathmini  ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2025/2026 pamoja usajili wa miradi kwenye  mfumo wa e -Delivery kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango Dkt Tausi Kida.

Bw. Kewe amebainisha kuwa tangu kuanza rasmi kwa mfumo huo Julai Mosi 2026 tayari miradi ya Maendeleo 150 kutoka taasisi na wizara mbalimbali imeshasajiliwa huku matarajio yakiwa kusajili miradi zaidi ya 500 ambayo inatakiwa kutekelezwa kwa kuzingatia Malengo na Shabaha za Dira 2050.

“mfumo wa e-Delivery ni mfumo wa kieletroniki ambao utafanya utekelezaji wa Dira 2050 kuwa wa ufanisi zaidi kwani unaongeza kasi ya uchambuzi wa miradi ya maendeleo na kutoa mrejesho pamoja na kurahisisha kufahamu idadi na aina ya miradi jambo litakalorahisisha kutoa vipaumbele kwenye miradi yenye matokeo makubwa katika utekelezaji wa Dira 2050” amesema Bw. Kewe.

e-Delivery ni Mfumo wa Kitaifa wa kusimamia Mipango na Miradi ya Maendeleo uliyounganishwa na mifumo mingine ya kitaifa ili kuongeza uwazi, uwajibikaji, ufanisi, na  usimamizi wa miradi ya maendeleo yenye matokeo makubwa kwa wananchi katika utekelezaji wa Dira 2050.