VIJANA NA DIRA 2050
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Mbaga Kida, amesema vijana ni nguvu kazi muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akiwataka kutumia ubunifu, teknolojia, utafiti na ujasiriamali kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii.
Dkt. Kida ameyasema hayo wakati akizungumza na vijana katika jukwaa la Wiki ya Ubunifu Tanzania 2026, lenye kauli mbiu kaulimbiu “Kutoka Kwenye Matarajio hadi Mabadiliko: Kutumia Ubunifu Kuelekea Tanzania yenye Ustawi wa Pamoja.”
Amesema Dira 2050 inaweka mwelekeo wa maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo, ikilenga Tanzania kufikia hadhi ya nchi yenye Uchumi wa Kipato cha Kati Ngazi ya Juu ifikapo mwaka 2050 kwa kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi, haki na linalojitegemea.
Amesema Dira hiyo imeainisha vichocheo vitano vya maendeleo na mageuzi ambavyo ni nishati, usafirishaji fungamanishi, sayansi na teknolojia, utafiti na maendeleo pamoja na mageuzi ya kidijitali, maeneo yanayowapa vijana nafasi kubwa ya kushiriki katika kujenga uchumi unaotegemea maarifa na ubunifu.
“Vijana hawapaswi kuonekana kama wanufaika wa maendeleo pekee, bali wanapaswa kuwa nguvu kazi, wabunifu, wajasiriamali na washiriki wakuu wa mageuzi ya kiuchumi na kijamii,” amesema.
Dkt. Kida amesema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji kizazi chenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kutumia teknolojia kubuni suluhisho, kuanzisha biashara, kufanya utafiti na kugeuza maarifa kuwa bidhaa na huduma zenye thamani.
Amesema malengo ya Dira yanatafsiriwa katika mipango ya Taifa ya muda mrefu, miaka mitano na mwaka mmoja ili kuhakikisha yanageuzwa kuwa programu, miradi, uwekezaji na matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Ametoa wito kwa vijana kutumia fursa za ubunifu, teknolojia, elimu na ujasiriamali kujijengea uwezo na kushiriki kikamilifu katika safari ya kuelekea mwaka 2050.