WABUNIFU WA NDANI WAELEZWA KUWA SULUHISHO LA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI
Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia Biashara na Ubunifu, Dkt. Blandina Kilama, amesema tafiti zenye shaidi na ubunifu ni njia bora ya kuleta suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo katika utekelezaji wa Dira 2050.
Dkt. Kilama amesema hayo wakati akitoa mada katika wiki ya Ubunifu Tanzania inayoendelea Jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza athari za mabadiliko ya tabianchi zinaonekana moja kwa moja katika jamii kupitia mabadiliko ya mifumo ya mvua, upungufu wa maji na kuvurugika kwa uzalishaji wa kilimo, hali inayosukuma jamii kubuni suluhisho kulingana na mazingira yao.
Amesema kama ambavyo miongoni mwa malengo ya Dira 2050 ni kujenga taifa linalostahimili mabadiliko ya tabianchi, ubunifu unaoonyesha uwezo wa kweli unaopaswa kuunganishwa na fedha, utaalamu, teknolojia, masoko na ushirikiano ili uweze kukua na kuleta matokeo.
Aidha Dkt Kilama ameongeza kuwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanapaswa kutambuliwa kama wabunifu na wajenzi wa suluhisho, huku maarifa ya jamii yakichanganywa na teknolojia mpya ili kutekeleza kwa ufanisi Dira 2050.
Hata hivyo ametoa wito kwa wadau kuhakikisha matokeo ya tafiti hayabaki kwenye ripoti, bali yafikishwe kwa watunga sera, wapangaji, wawekezaji na watekelezaji huku wadau wote wakiimarisha ushirikiano, kuondoa vikwazo na kuwekeza katika ubunifu unaoweza kuboresha maisha ya wananchi na kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
Wiki ya Ubunifu Tanzania inayoendelea jijini Dar es salaam imebeba kauli mbiu isemayo “From Local Innovation to Impact: Advancing Inclusive Climate Solutions to Scale.”