Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

UTEKELEZAJI WA DIRA 2050 KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU
06 Aug, 2026
UTEKELEZAJI WA DIRA 2050 KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU

Tanzania imesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utaongeza kasi ya kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kuyajumuisha kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb), Julai 13, 2026, alipohutubia kwneye Mdahalo Mkuu wa Jukwaa la Siasa la Ngazi ya Juu la Umoja wa Mataifa la Utekelezaji wa Maendeleo Endelevu (HLPF) unaoendelea jijini New York-Marekani.

Akiwasilisha tamko la Tanzania, Prof. Mkumbo amesema licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi, misukosuko ya uchumi na migogoro ya kikanda, nchi imeendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa SDGs, ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi, huduma za afya, elimu bora, umeme, mageuzi ya kidijitali, uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati, pamoja na uhamasishaji wa rasilimali za ndani na kuimarika kwa taasisi za umma.

Ameeleza kuwa Agenda 2030 imeunganishwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), hatua itakayoweka msingi wa kuendeleza utekelezaji wa SDGs hata baada ya mwaka 2030. 

Vipaumbele vya kipindi kijacho ni kilimo cha kisasa, viwanda, uchumi wa buluu, ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, mageuzi ya kidijitali, maendeleo ya rasilimali watu na uhamasishaji wa rasilimali za ndani.

Aidha Prof. Mkumbo ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kikamilifu Azimio la Siasa la Umoja wa Mataifa la mwaka 2023 na kuunga mkono mpango wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa SDG Stimulus, ikiwemo kupunguza riba za mikopo, kushughulikia changamoto za madeni, kuongeza upatikanaji wa mikopo nafuu ya kugharamia miradi ya maendeleo na kuharakisha mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa ili uwe jumuishi na unaozijali zaidi nchi zinazoendelea.

Kesho, Julai 14, 2026, Tanzania itawasilisha rasmi Taarifa yake ya Tatu ya Mapitio ya Hiari ya Utekelezaji wa SDGs (Third Voluntary National Review – VNR).